Mahari yangu ilirejeshwa kutokana na utasa

Last Updated on 13/10/2021 by Tabibu Fadhili Paulo

Roseline Orwa ni mama wa miaka 46, yeye ni mwanamke mjane ambaye hakufanikiwa kushika mimba wakati wa ndoa zake mbili , ila hilo halijamkosesha usingizi kwa kukubali hali yake.

Baada ya yeye kuamua kuwa, licha ya changamoto ya kuwa hana uwezo wa kushika mimba basi amewarithi watoto mayatima na kuwalea kama Watoto wake.

Kwa hivi sasa ana watoto 27 chini ya wakfu alioufungua wa Rona Widows and orphans center uliopo eneo la Bondo nchini Kenya .

Akiwa bado na miaka yake ya 20 na kitu hivi, Rosaline alikuwa na tamaa na njaa kuu mno ya kupata ujauzito , aghalab hii ndio hali ya wanawake wengi hasa wanapoingia katika ndoa.

Ikiwa pia kukiwa na shinikizo kuu kutoka kwa shemeji zake na pia kutoka kwa aliyekuwa mume wake wa kwanza ila shinikizo kubwa lilitokana na yeye mwenyewe alihisi kana kwamba hakutosha mboga ikiwa hajajifungua mwana katika jamii yake .

“Nikitizama nyuma ninaona kana kwamba asilimia zaidi ya mia moja , nilikuwa na shauku ya hali ya juu ya kushika mimba , mimi ni wale mabinti wa kutoka vijijini ambao huamini kuwa thamani ya mwanamke ambaye ameingia kwenye ndoa ni uwezo wake wa kupata mtoto “anakumbuka Roseline.

Mwanamke huyu anasema kuwa mawazo na dhana alizokuwa nazo zilitokana na maoni ya wengi katika jamii yake na kwa hio msukumo aliokuwa nao ni mkubwa mno .

Ndoa ya kwanza na hatma yake

Roseline Orwa

CHANZO CHA PICHA, ROSELINE ORWA

Njaa na ari yake ya kujaliwa mtoto ilimsukuma kujaribu matibabu mbalimbali katika kutafuta jawabu la kuwa mama.

Hivyobasi katika kipindi cha miaka mitatu aliokuwa kwenye ndoa yake ya kwanza Rosaline alipitishwa kwenye upasauaji mara tatu .

“Nilikuwa nimepatikana na matatizo ya ugonjwa wa Endometrioisis , kando na hayo mirija yangu ya kizazi ilikuwa imefungana , kwa hio nilitafuta majibu kutoka kwa madaktari mbalimbali wa afya ya kizazi miongoni mwa wanawake .

Waliposhindwa kunihudumia kwa njia ambayo ilitoa majibu ya kushika mimba , nilijipata nikitafuta usaidizi kutoka kwa matibabu ya kienyeji “anakumbuka Rosaline.

Ni hali ambayo ilimkosesha usingizi , Suala lililosababisha misukosuko katika ndoa yake .

Ilikuwa bayana kuwa ndoa ilikuwa imefika ukingoni kutokana na shida zake za kupata ujauzito .

Ilikuwa huzuni kuwa ndoa yake ilifika ukingoni kutokana na changamoto yake ya kushika mimba , ila kilichoumiza zaidi ni kuwa katika ndoa ya pili na bado hakuna mtoto.

Rosaline

CHANZO CHA PICHA,ROSALINE

Rosaline aliingia kwenye ndoa ya pili , ila wakati huu hakukuwa na shinikizo kuu hasa kutoka kwa mume wake . Rosaline anasema kuwa hata kabla ya yeye na mume wake wa pili kukubaliana juu ya ndoa , tayari alikuwa amemueleza kuhusiana na changamoto yake ya kuwa tasa .

Japo kama kawaida na njaa aliokuwa nayo ya kuwa mama , aliendelea kuhangaika akitafuta mbinu za kushika mimba ila aliambulia patupu .

“Kitu ambacho kilikuwa tofauti na mume wangu wa pili ni kuwa alisimama na mimi , wakati watu wa jamii yake waliponiinukia kuhusu swala la ni kwanini sikuwa na uwezo wa kushika mimba “anakumbuka Roseline.

Rosaline alikuwa ni kitindawili kati ya ndugu na dada zake , anasema kuwa kati ya kaka na dada wake ni yeye pekee yake aliyekuwa hajajaaliwa mtoto .

“Jamii ya kikwetu huamini kuwa wanawake kama mimi ambao wanakuwa na tatizo la kujaaliwa watoto wanajulikana kwa jina LUR ikimaanisha mti ambao hauna uwezo wa kuzaa tunda , majina kama haya unapotwikwa wakati una utasa yanauma mno , ile hali ya wanawake kama sisi wanaipitia katika jamii tunazoishi ni ya machungu sana “Rosaline anasema.

Rosaline

CHANZO CHA PICHA,ROSALINE

Uchungu na mahangaiko ya kutoshika mimba akiwa kwenye ndoa ilimkosesha amani Bi .Rosaline ikawadia wakati ambapo aliwazia kujitoa uhai wake , Mwanamke huyu anasema kuwa katika mazingira ya anakotoka wanawake kama yeye huonekana kama jangwa na wasiofaa , ni maoni na mawazo kama hayo yaliompatia wazo la kukosa kujidhamini .

Mwaka wa 2009 mume wake wa pili alifariki baada ya kuugua , habari za kufariki kwa mume wake zilimpa sonona asijue la kufanya ,kwani katika ndoa ya pili alihisi kulindwa na kupendwa.

Kifo cha mume wake kilimaanisha kuwa baada ya kipindi cha maombolezo na mazishi , ingembidi kurejea kwao nyumbani kutokana na kuwa hakuwa amejaaliwa mtoto.

Ilikuwa ni mara ya pli Rosaline alirudi nyumbani kwao, kwa bahati nzuri anasema kuwa mama yake mzazi amekuwa nguzo muhimu kwani alimpokea bila kumbagua.

Kipindi hiki alichokaa nyumbani baada ya kuwa mjane aliamua kutafuta mbinu ya kuitwa mama bila kujifungua mtoto .

Mwaka wa 2012 miaka minne baada ya mumewe kuaga dunia alianza wakfu wa Rona unaoshughulikia watoto yatima.

Yeye pamoja na wanawake wengine wanane ambao walikuwa wajane walianza shughuli ya kukutana na kuzungumzia changamoto zao za kila siku.

Katika pilka pilka hizo alianza kuzungumzia hali yake ya utasa .

Rosaline aligundua kuwa kulikuwa na wanawake wengi ambao walikuwa wameficha hali kama yake kutokana na unyanyapaa katika jamii .

Rosaline

CHANZO CHA PICHA, ROSALINE

“Kwa muda mrefu sikuwa tayari kuzungumza wazi wazi kuwa mimi nilikuwa tasa , kwani hali kama hii inaandamana na uchungu sana , hali yangu ya kutamani watoto ilizidi chochote nilichokuwa duniani na ndipo saa moyo wa kuwarithi watoto yatima lilinijia “anasema Rosaline

Kupitia wakfu huo Rosaline kwa sasa amewarithi watoto 27 ambao wako kati ya umri wa miaka 8 na 18.

Kwake yeye anasema kuwa amefunga midomo ya wengi ambao walimsema na kumyooshea kidole cha lawama kwa kuwa tasa , kwani kwa rehema za kudura ana midomo 27 ya kutafutia chakula na hilo kwake ni ndoto tosha

“Nilikubali hali yangu ya utasa , lakini fahari yangu kuu ni kuitwa mama na kupewa fursa ya kuwalea na kuwapa upendo hawa wana wangu 27” Rosaline anasema.

source

Imesomwa na watu 304
Mahari yangu ilirejeshwa kutokana na utasa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *