Last Updated on 03/11/2021 by Tabibu Fadhili Paulo
Jinsi ya kuishi inapogundulika huna uwezo kabisa wa kupata mtoto
Umeshatafuta mtoto kwa miaka mitatu, kwa miaka mitano au hata miaka kumi na hakuna dalili zozote kama utakuja kumpata.
Mmeshapima kila hospitali na imegundulika wazi hakuna uwezekano tena wa kupata ujauzito.
Pengine mmeshatumia dawa mbalimbali toka hospitali mbalimbali na bado hampati ujauzito.
Mmeshajaribu hata dawa za asili toka kwa wataalamu mbalimbali wa tiba asili lakini bado mambo yamegoma.
Kama ni maombi mmeshafanya hadi mikesha mbalimbali ya manabii na mitume mmehudhuria lakini bado hakuna ujauzito.
Mmekata tamaa, mmeishiwa pozi na mmeamua kuishi kwa mawazo mawazo tu kila kukicha.
Nipo hapa kukuambia bado maisha yanatakiwa yaendelee.
Bado unatakiwa uendelee kuishi na bado jamii na taifa tunakuhitaji.
Sipo hapa kukuambia kwamba hilo ni jambo rahisi tu na kwamba unatakiwa utabasamu tu na kwamba hilo ni tatizo dogo tu.
HAPANA.
Nipo hapa kukuambia mwenye tatizo kama lako siyo wewe tu peke yako, wapo wengine wengi sana wana tatizo kama lako lakini wamelipokea na wameamua kumwachia Mungu ili kuruhusu maisha mengine yaendelee.
Kwenye maisha kila mtu anahangaika na jambo fulani na hakuna mtu asiye na shida au kikwazo fulani.
Wakati wewe unahangaika kutibu mafua kuna mwingine anahangaika kutibu saratani.
Wakati wewe unahangaika kupata viatu vya kuvaa mwingine hata hiyo miguu hana alipata ajali na kulazimika kukatwa miguu.
Usiruhusu tatizo lolote unalopitia au unaloishi nalo liwe kuuuubwa kuliko hata Mungu wako.
Kama bado upo hai basi tegemea kukutana na tatizo hili na lile kwenye safari yako ya kuishi.
Matatizo yote yanayokusumbua yataisha na kupotea yenyewe siku tu ukifa.
Jinsi ya kuishi inapogundulika huna uwezo kabisa wa kupata mtoto
1. Mwachie Mungu yote
Kuna mambo mengi tu kwenye maisha yetu hayaelezeki na ni vigumu kumwambia mtu na akakuelewa.
Kuna mtu anamaliza tu shule tayari ameshapata kazi, mwingine anamaliza shule anahangaika miaka hata 10 hapati kazi.
Unapokutana na mambo ambayo kwa akili za kibinadamu ni ngumu kuyaelewa unatakiwa umuachie Mungu na uendelee na maisha yako mengine.
Najua siyo rahisi kulipokea hili lakini kwa usalama wa akili na nafsi yako nakusisitiza umuachie tu Mungu.
Hatuwezi kuelewa kila linalotutokea maishani linatokea kwa sababu gani.
Kumbuka pamoja na kwamba umehangaika sana kutafuta mtoto na imeshindikana haina maana ndiyo mwisho wa dunia.
HAPANA.
Ukichunguza vizuri utaona kwamba hakuna mtu ambaye anacho kila anachokihitaji kwenye maisha yake.
Inawezekana wewe huna mtoto lakini gari unalo.
Mwingine ana mtoto lakini hata boda boda hana.
Mwingine ana mtoto lakini huyo huyo mtoto ni chanzo cha shida kwenye maisha yake; ni mtoto mkorofi, mwizi, mlevi wa kupindukia, amesababisha wazazi kukopa mamilioni ya pesa ili kumsomesha na bado aliferi masomo.
Kwahiyo haijalishi unawaza nini juu ya hali yako ya kutopata mtoto, bado unayo mengi tu ya kumshukuru Mungu
2. Acha kujilaumu mwenyewe
Inawezekana umesubiri muda mrefu sana upate mtoto na uwe na familia yako.
Inawezekana mambo fulani uliyofanya ulipokuwa shuleni au chuoni ndiyo yamepelekea kuharibu kizazi chako.
Labda muda mwingi kwenye ujana wako ulikuwa unakula vyakula visivyofaa hata vikapelekea uharibifu kwenye afya yako ya uzazi.
Inawezekana pia hujuwi ni nini hasa ndiyo sababu ya haya yote.
Pamoja na hayo yote bado nakushauri uache tabia ya kujilaumu na kuhuzunika kila siku.
Wakati mwingine kuendelea kujilaumu na kuhuzunika hakuondoi wala kupunguza tatizo bali kunafanya tatizo kuwa kubwa zaidi bila mwenyewe kujua.
3. Usiishi kwa kufuata maneno ya watu
Hapa ndipo shida ya kila kitu inapoanzia.
Bila kusikiliza watu wanasemaje juu yako au wanakuonaje ndiyo jambo la mhimu ili uishi maisha yako ya uhuru na furaha.
Chanzo cha matatizo mengi kwenye maisha yetu ni kusikiliza watu wengine wanasemaje juu ya maisha yako.
Mimi hapa kwa mfano nina zaidi ya mwaka sasa nina suruali moja tu.
NDIYO nina suruali moja tu, navaa hiyo kila siku asubuhi mchana na jioni.
Nikivua navaa kaptula naifua hiyo suruali yangu moja ikikauka navaa tena.
Kuna wanaonishangaa kwa kuwa na suruali moja. Kuna wanaodhani labda ni masharti nimepewa na mganga wa kienyeji, kuna wanaosema mimi ni bahili sana na kuna wanaodhani huenda mimi ni chizi.
Lakini mimi nipo salama, nalala vizuri, nakula vizuri na sina hofu yoyote ya kuwa na suruali moja kila siku.
Ni maamuzi yangu, ni maisha yangu nimechagua mwenyewe.
Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa hilo tatizo la kushindwa kupata mtoto huenda shida hasa siyo wewe bali ni ndugu, jamaa na marafiki ndiyo wanaokufanya uwe na mawazo mawazo na huzuni zisizoisha kisa tu huna mtoto.
Ndoa siyo watoto tu wala ndoa siyo tendo la ndoa tu kama wengine wanavyodhani.
Kuna mengine mengi ya mhimu kwenye ndoa zaidi ya watoto na tendo la ndoa.
Acha kuwasikiliza watu wanasemaje, waache waongee watakavyo lakini wewe endelea na maisha yako.
Huwezi kuwazuia watu wasiongee kuhusu wewe hata ungekuwa vipi lazima kwa namna moja au nyingine watakusema tu hata uweje.
Watu wanamsema hadi marehemu, itakuwa wewe uliye hai?
Ishi maisha yako mwenyewe na hata siku ukifa utazikwa mwenyewe peke yako.
4. Omba mtoto mmoja yatima uishi naye
Kama shida yako hasa ni kuwa na mtoto tu unayeweza kumpenda, kumtunza na kumsomesha siyo lazima awe wa kumzaa mwenyewe.
Kama upo tayari unaweza kwenda kwenye kituo cha watoto yatima na uombe kupewa mtoto mmoja au hata wawili na ukae nao.
Shida ni nini hasa kwani? Mambo yasiwe mengi sana nenda kituo cha watoto yatima upewe mtoto endelea na maisha yako.
Kama unaona shida kumchukuwa mtoto yatima angalia kati ya ndugu zako au hata rafiki zako kuna mmoja ana mtoto au watoto ambao hata hawezi kuwamudu wote vizuri, omba wakupe mmoja na uishi naye.
Kwa njia hii tu huenda Mungu akaona nafsi yako ilivyo njema na hata kwa namna za kimiujiza ukashangaa umepata ujauzito na wewe.
Miujiza ipo maishani, usiwe kipofu.
5. Endelea kufurahia maisha
Kutopata mtoto isiwe ndiyo mwisho wako wa kutabasamu na kufurahia maisha mengine kwa ujumla.
NDIYO nafahamu ni jambo linaloumiza lakini kama nilivyokuambia hapo juu kila mmoja wetu ana jambo fulani ambalo halijakaa sawa kwenye maisha yake lakini hilo halifanyi nishindwe kutabasamu, nishindwe kunywa soda au nishindwe kwenda kusalimia marafiki zangu na kwenda uwanja wa taifa kushangilia timu yangu ya Yanga inapocheza.
Maisha lazima yaendelee.
Hata niwe na watoto 100 bado nakumbuka nilizaliwa peke yangu na nitazikwa peke yangu.
Kuna mambo mengine mhimu unaweza kuendelea nayo, natakiwa kushughulika na kazi yangu au biashara yangu, natakiwa kufuatilia masomo yangu, natakiwa kuwahudumia wazazi wangu na ndugu zangu wengine wasio na msaada na mengine mengi.
Mungu hakunileta duniani ili kuzaa tu, hapana, nina mengine mengi naweza kufanya zaidi ya hayo ya kuzaa.
Kwanza dunia tayari inakabiliwa na ongezeko kubwa la watu ambalo ni tishio kwa ustawi wa dunia.
Miaka ya sasa ikitokea nafasi 3 tu za kazi zimetangazwa utashangaa watu 10000 wametuma maombi ya kazi!
Kwa hiyo usiache kuwa na furaha, usiache kwenda disko wala usiache kuendelea kushiriki na kufurahia tendo la ndoa kisa tu huna mtoto.
Una mengine mengi ya kumshukuru Mungu.
Hata kuwa hai tu hujalazwa hospitali ni jambo la kumshukuru Mungu.
Kuna mtu amelazwa hospitali miezi na miezi na hajuwi ataruhusiwa lini kutoka na bado bili zinazidi kusoma na hajuwi atapona au la.