Last Updated on 28/11/2021 by Tabibu Fadhili Paulo
Vyakula na vinywaji 11 ambavyo mama mjamzito hatakiwi kula.
Kitu cha kwanza kabisa unachotakiwa kujifunza mara tu unapopata ujauzito ni kufahamu vyakula na vinywaji ambavyo hutakiwi kula.
Bila kuwa makini wakati huu unaweza kukutana na matatizo mengi yanayotokana na ujauzito ikiwemo ujauzito wenyewe kukutoka.
Hakuna kitu kinaumiza kama mtu umehangaika kutafuta ujuauzito kwa miezi kadhaa na wakati mwingine hata miaka kadhaa, wakati mwingine ilikulazimu hata kuingia gharama kununua dawa ili kupata ujauzito; halafu inatokea bahati unaupata LAKINI ndani ya mwezi mmoja au miwili ujauzito unakutoka!
Mara nyingi huwa ni matokeo ya kutofahamu nini hasa hutakiwi kula wakati ukiwa mjamzito.
Shida inaweza kuwa kubwa kama mama anatumia aina fulani za vilevi au kilevi na ni mlevi sana wa kupindukia.
Bahati nzuri ni kuwa ukiwa ni mtu wa kupenda kujisomea utaona kuna vyakula vingi zaidi unavyoweza kula ukiwa mjamzito kuliko vile ambavyo unakatazwa kula.
Unatakiwa uwe makini sana sana wakati huu ukiwa mjamzito juu ya nini unakula na kunywa ili wewe mwenyewe ubaki na afya nzuri, uwe na ujauzito usio na misukosuko ya kuumwa kila mara na mhimu zaidi mtoto aliyoko tumboni naye awe na afya nzuri na akizaliwa awe pia na afya nzuri ya mwili hata na akili.
Ulivyo wewe ni kile unachotumbukiza mwilini mwako kila siku.
Baadhi ya vyakula utatakiwa ule mara chache sana na vingine utatakiwa uviache kabisa hata kama unavipenda.
Kumbuka nazungumzia vyakula na vinywaji ambavyo mama mjamzito hatakiwi kula. Kama wewe siyo mjamzito unaweza kuendelea kuvitumia.
Vyakula na vinywaji 11 ambavyo mama mjamzito hatakiwi kula;
1. Samaki wenye madini mengi ya Zebaki.
Zebaki (Mercury) ni sumu kubwa.
Mara nyingi zebaki inapatikana kwenye maji yaliyochafuliwa.
Kwahiyo kama unakula samaki wa maji chumvi na baharini zinakovuliwa hizo samaki kuna uchafuzi wa mazingira kuna uwezekano mkubwa samaki unaokula wana sumu hii ndani yake.
Kama utakuwa unakula mara nyingi samaki wa maji chumvi wenye sumu hii zebaki iliyomo ndani yao inaweza kudhuru mfumo wako wa fahamu, mfumo wako wa kinga ya mwili na kudhuru figo.
Samaki hao wanaweza pia kuleta shida kwenye ukuwaji wa mtoto na afya ya mtoto kwa ujumla.
Mtoto akizaliwa anakuwa hana afya nzuri, hakui kwa haraka na anakuwa ni mdhaifu tu kwa ujumla.
Kwa sababu sumu hii inapatikana kwenye bahari ambayo ni chafu basi samaki wakubwa wa baharini ndiyo wenye kiwango kikubwa zaidi cha sumu hii kuliko samaki wa baharini wadogo wadogo.
Kwahiyo ni jambo la afya kuepukakula samaki wenye zebaki kwa wingi wakati wa ujauzito na hata wakati wa kunyonyesha.
Samaki wanaoaminika kuwa na zebaki kwa wingi ni pamoja na wafuatao:
shark
swordfish
king mackerel
tuna (especially bigeye tuna)
marlin
tilefish from the Gulf of Mexico
orange roughy
Vile vile ni mhimu kufahamu kuwa siyo samaki wote wa baharini wana hii zebaki kwa wingi.
Ni baadhi yao tu na siyo wote.
Kuna samaki wengine wana kiasi kidogo sana cha zebaki ambacho ni salama na kama unakula mara moja moja samaki hao hakuna madhara yoyote utayapata.
Samaki wenye kiasi kidogo sana cha zebaki na bila madhara ni pamoja na:
dagaa maalumu wa kwenye kopo wenye chumvi (anchovies)
chewa (cod)
flounder
haddock
samoni (samaki mkubwa mwenye mnofu mwekundu) > salmon
tilapia
trout (freshwater)
Unatakiwa upendelee kula zaidi samaki wenye mafuta na omega 3 kwa ajili ya afya bora kabisa ya ujauzito na afya ya mtoto kwa ujumla.
Samaki wenye omega 3 kwa wingi ni pamoja na salmon na anchovies.
2. Samaki ambao hawajaiva vizuri
Hii inaweza kuwa ngumu sana hasa kama wewe ni mpenzi wa sushi.
Samaki ambao hawajaiva vizuri au wabichi wanaweza kukusababishia maambukizi yanayohusianayo na bakteria au hata virusi kama wewe ni mjamzito.
Bakteria na virusi hao unaoweza kuwapata kwa kula samaki amabye hajaiva vizuri ni pamoja na norovirus, Vibrio, Salmonella,na Listeria.
Baadhi ya hayo maambukizi yanaweza kukupata wewe tu na mengine yanaweza kumfikia hadi mtoto aliyopo tumboni; unaweza kupatwa na madhara kama ya kuishiwa maji mwilini na udhaifu tu wa mwili kwa ujumla.
Wanawake wengi wajawazito mara nyingi wanapata maambukizi ya bakteria aitwaye listeria.
Bakteria huyu anapatikana kwa wingi kwenye udongo au kwenye maji amabayo si masafi na salama au kwenye mimea.
Ingawa sisi waafrika na watanzania kwa ujumla hatuna pishi hili la samaki ambaye hajapikwa, wazungu wanakula samaki ambaye hajapikwa ambaye huandaliwa maalumu na huitwa ‘sushi’, kwenye mahoteli ya kitalii hata hapa Tanzania ukienda mlo huu upo.
Sushi au samaki ambaye hajapikwa anaweza kuingiwa na hawa bakteria au virusi wakati wa kumuandaa.
Bakteria Listeria anaweza kumwingia mtoto aliyopo tumboni kupitia kondo la nyuma wanaita placenta na inaweza kutokea hivyo hata kama mama mjamzito haonyeshi dalili yoyote ya kuumwa.
Bakteria huyu anaweza kuleta matatizo kama vile mtoto kuzaliwa kabla ya miezi 9 (njiti), mimba kutoka kila mara na matatizo mengine mengi ya kiafya kwa mama mjamzito.
Hivyo ukiwa mjamzito hakikisha kama unakula samaki basi awe amepikwa na ameiva kabisa na unaweza kuendelea kula sushi baada ya kujifungua.
3. Kaffeina
Kama wewe ni mpenzi wa kahawa, chai ya rangi, soda za energy, au cocoa; utakapokuwa mjazmito utatakiwa kuviepuka hivi au kuvipunguza sana.
Mwanamke mjamzito anashauriwa kutokunywa chochote chenye kaffeina ndani yake zaidi ya mililita 200 kwa siku na atakayeweza kuviepuka kabisa ni vizuri zaidi.
Kaffeina inameng’enywa haraka sana na mwili wa mama na inaweza kupenya na kumfikia mtoto kirahisi zaidi.
Shida ni kwamba mtoto akiwa tumboni bado hana vimeng’enya vinayoweza kumsaidia kuimeng’enya hii kaffeina kwa haraka na hivyo kaffeina inaweza kujirundika kirahisi ndani ya mwili wa mtoto.
Unywaji uliozidi wa vinywaji vyenye kaffeina unaweza kuingilia ukuwaji mzuri wa mtoto tumboni na kupelekea mtoto kuzaliwa na uzito pungufu.
Mtoto anapozaliwa na uzito pungufu yaani chini ya kg 2 na nusu anakuwa kwenye hatari ya kufa mapema bado mchanga na akibahatika akawa mkubwa huwa mhanga wa magonjwa sugu yasiyopona kwa haraka.
Kwahiyo ili kurahisisha kipengele hiki nakushauri ukiwa mjamzito usinywe kabisa soda yoyote, usinywe juisi yoyote ya dukani, usinywe kahawa, chai ya rangi na cocoa.
4. Pombe
Inashauriwa kuacha kabisa kunywa pombe wakati ukiwa mjamzito.
Na siyo pombe tu hili linaenda sambamba pia kwa vilevi vingine vyote.
Pombe na vilevi vingine kama sigara, bangi na madawa mengine ya kulevya yanaweza kukuletea tatizo la mimba kutoka kila mara unapoipata.
Hata kiasi kidogo tu cha pombe bado kinaweza kuathiri afya ya ubongo wa mtoto aliyopo tumboni.
Hata kama una arosto kiasi gani, kama una ujauzito jizuie tu kwa ajili ya usalama wa mtoto.
Unaweza kuendelea na mambo yako baada ya kumaliza kunyonyesha.
5. Vyakula feki
Vyakula feki hujulikana kwa kiingereza kama ‘Processed junk foods’.
Kwa lugha nyepesi hivi ni vyakula vya kwenye makopo vya dukani au kwenye migahawa ya fast foods.
Wakati unapokuwa mjamzito ndiyo wakati hasa wa kugeukia kula vyakula vya asili zaidi kwa ajili yako na kwa ajili ya afya ya mtoto kwa ujumla.
Utahitaji kuongeza zaidi vyakula vya asili vyenye viinilishe mhimu kama vyenye protini hasa protini ya kwenye mimea na siyo nyama, vyakula vyenye madini ya chuma, madini ya folate na choline.
Vile vile kuna dhana potofu kuwa ukiwa mjamzito basi unakuwa unakula kwa ajili ya watu wawili hivyo unatakiwa kula zaidi; hili siyo kweli.
Bado unaweza kuendelea kula kawaida hata kama una ujauzito hasa katika miezi mitatu ya mwanzo na baadaye unaweza kuongeza kidogo ndani ya miezi 6 na kuongeza kidogo zaidi tena ndani ya miezi mitatu ya mwisho.
Vyakula feki mara nyingi huwa havina viinilishe mhimu ndani yake, vina kalori nyingi zaidi ambazo mwili hauzihitaji, vina sukari kupita kiasi tena mara nyingi siyo sukari ya asili inayotumika kuviandaa bali ni sukari ya viwandani (artificial sweeteners) na huongezwa mafuta zaidi.
Vyakula hivi vinaweza kupelekea mama akaongezeka sana uzito, akapata kisukari, na matatizo mengine wakati wa kujifungua.
vyakula vingine mama mjamzito anashauriwa kutokula akiwa mjamzito ni pamoja na;
6. Nyama ambayo haijaiva vizuri
7. Matunda na mboga ambavyo havijaoshwa au kusafiswa vizuri
8. Maziwa ambayo hayajachemshwa
9. jibini (cheese)
10. Kachumbari
11. Mayai ambayo hayajapikwa ikiwemo mayonaise iliyotengenezwa nyumbani
Ukipata muda soma na hii > Chakula cha mama mjamzito
Ikiwa unatafuta dawa ya asili ili kupata ujauzito niachie tu ujumbe WhatsApp +255714800175