Last Updated on 06/02/2023 by Tabibu Fadhili Paulo
Sababu za kupoteza hamu ya kula wakati wa ujauzito
Wapo baadhi ya wanawake wajawazito wamekuwa wakinitafuta na kuniuliza kwanini wanaishiwa au wanapungukiwa na hamu ya kula chakula.
Wengi wao wanasema tatizo hilo hawakuwahi kuwa nalo kabla ya kuwa na ujauzito.
Basi kwenye makala hii nitajadili kwa kirefu juu ya sababu ya kupungua hamu ya kula wakati wa ujauzito na nini unaweza kufanya ili kukabiliana na tatizo hilo linapojitokeza.
Kwanza kabisa tambua kwamba ni mhimu sana kushughulika na tatizo hili mapema linapojitokeza kwa sababu ujauzito unahitaji mama apate chakula kingi na cha kutosha ili kusaidia ukuaji mzuri wa mtoto aliyopo tumboni.
Kupungua kwa hamu ya kula wakati wa ujauzito kwa sehemu kubwa ni matokeo ya mabadiliko ya kihomoni yanayokuja kama matokeo ya ujauzito ulionao.
Ili kulinda afya yako na ya mtoto mtarajiwa, ni mhimu kwamba unachukua hatua stahiki ili kurejesha hamu yako ya kula chakula.
Hata hivyo ni mhimu kuzingatia kula chakula sahihi na maalumu kwa ajili ya mama mjamzito na siyo kula tu chakula chochote kwa lengo la kushiba.
Unapokuwa mjamzito ni jambo la kawaida kiwango cha njaa yako kushuka au kuongezeka mara kwa mara kama mabadiliko unayoyapata sababu ya ujauzito.
Utajikuta unapoteza tu hamu ya kula chakula chochote na wakati mwingine unaweza kupoteza hamu kwa baadhi ya vyakula.
Kuna sababu kadhaa zinazoweza kupelekea ukapoteza hamu ya kula wakati wa ujauzito ambazo ni pamoja na zifuatazo ;
1. Uchovu wa mwili na akili
2. Kutapika kwa mara kwa mara
3. Msongo wa mawazo
4. Baadhi ya dawa
5. Mabadiliko ya homoni
6. Kiungulia
7. Kuchelewa kupata choo
8. Uvimbe tumboni
Hizo ni baadhi ya sababu ambazo zinaweza kupelekea mama mjamzito kupoteza hamu ya chakula wakati wa ujauzito.
Vitu vya kufanya ili kurudishia hamu ya chakula wakati wa ujauzito
Unaweza kufanya mambo yafuatayo ili kurudishia hamu yako iliyopotea ya kula chakula
1. Kula chakula kidogo mara nyingi
>Jaribu kula chakula kidogo au chakula kichache mara nyingi katika siku badala ya kula chakula kingi kwa wakati mmoja.
2. Kula zaidi chakula unachokipenda
>Kuna chakula fulani katika vyakula vilivyopo nyumbani ambacho unakipenda zaidi kuliko vingine. Jaribu kula zaidi chakula hicho.
3. Epuka vyakula feki
>Wakati wote wa ujauzito ni mhimu kwamba unaweka mkazo kwenye kula vyakula sahihi na vyenye afya maalumu kwa ajili ya mama mjamzito.
Vyakula feki ni vyakula vya kwenye makopo au vyakula vya viwandani na vya kwenye migahawa (fast food).
Jiwekee mazoea ya kula vyakula vya asili zaidi hasa wakati huu unaposumbuliwa na tatizo la kukosa hamu ya kula.
4. Jaribu tangawizi
>Tangawizi ni dawa ya asili ya kuongeza hamu ya chakula kwa mama mjamzito
>Faida nyingine ya tangawizi ni kukuondolea homa za asubuhi wakati wa ujauzito na itakusaidia pia kuzuia hali ya kutapika ambayo huwatokea wakinamama wengi wajawazito hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito.
>Unaweza kunywa chai ya tangawizi kikombe kimoja (robo lita) kutwa mara 2 asubuhi na jioni.
>Tafadhali usinywe tangawizi nyingi kupita kiasi kwani inaweza kusababisha ujauzito kutoka hasa ujauzito wa chini ya miezi miwili.
5. Jaribu vyakula vingine vipya
>Usiwe mtu wa kukariri kula chakula fulani tu hicho hicho kila siku.
>Jaribu vyakula vingine vipya tofauti na ulivyozoea. Ladha mpya nyingine ya chakula kipya inaweza kukusaidia kutamani kula zaidi. Na usisahau kula chakula sahihi.
6. Fanya mazoezi ya viungo
>Kama wewe ni mtu wa kula na kulala au kula na kukaa tu kwenye kiti unaangalia TV unaweza kupata tatizo la kupungukiwa hamu ya kula kirahisi zaidi.
>Kuna baadhi ya wanawake hata wanaume wanaamini mwanamke akiwa mjamzito basi anatakiwa kula na kukaa tu bila kujishughulisha na chochote, hali hii ni moja ya sababu za kupoteza hamu ya kula chakula.
>Kama ujauzito wako hauna shida yoyote na hujaandikiwa mapumziko maalumu na daktari (bed rest), basi ni mhimu mama mjamzito uwe mtu wa kujishughulisha na mazoezi ya viungo madogo madogo ya hapa na pale kama vile kutembea kwa miguu na kusimama mara moja moja.
>Tafadhali sana usifanye mazoezi mazito na magumu wakati wa ujauzito, ni mhimu kumshirikisha daktari wako wa karibu juu ya mazoezi gani hasa ni mazuri kwako wakati huu wa ujauzito.
Naomba niishie hapa kwa leo
Kama una swali zaidi uliza hapo chini kwenye boksi la comment na mimi nitakujibu
Na kama kuna mtu anahangaika kupata ujauzito na anatafuta dawa ya asili ya kumsaidia kupata ujauzito basi niachie tu ujumbe WhatsApp +255714800175